Ndugu wanahabari,

Tarehe 29 Juni 2017 Serikali ya Tanzania iliwasilisha miswada mitatu bungeni inayohusu sekta ya uziduaji kwa “Hati ya Dharura.”  Miswada hiyo ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017; Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017; na Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2017.

Kwa msingi huu,  HakiRasilimali-PWYP, tulikutana Dar es salaam tarehe 30 June na kufanya uchambuzi wa miswada hiyo na kufikia maazimiio yafuatayo.

TUNAIPONGEZA serikali kwa uamuzi wa kuwasilisha bungeni miswada hii tajwa hapo juu

Na kwa uthubutu na msimamo wa kuhuisha upya mjadala wa kitaifa kuhusu usimamizi wa rasilimali za nchi na manufaa yake kwa taifa.

 

HOFU YETU: Uharaka wa kupitisha miswada hii, haujawezesha ushiriki mpana wa wadau na wananchi wa ujumla, uchambuzi wa kina na mjadala wa kutosha. Uzoefu unaonyesha utaratibu kamaa huu haupelekei kupatikana kwasheria nzuri kama ilivyofanyika mwaka 1998, 2010 na 2015.

 

Ndugu wanahabari,

TUNAWASIHI wabunge kupitia miswada hii kwa uangalifu na kutanguliza mbele maslahi mapana ya Taifa.

 

MUSWADA WA SHERIA YA MAPITIO NA MAJADILIANO KUHUSU MASHARTI HASI KATIKA MIKATABA YA MALIASILI ZA NCHI WA MWAKA 2017

 

  • Jamii na kila raia wa Tanzania sio kipaumbele kwenye mabadiliko na mapendekezo mapya katika sheria hii ambapo sauti na matamanio ya watanzania hayajatiliwa maanani.

 

  • Ieleweke kwamba kifungu cha nne kifungu kidogo kwa kwanza, kinalipatia bunge hiari ya kufanya mapitio ya mikataba. Hii inaweza isifanyike. Sisi tunashauri bunge lipewe mamlaka ya kupitia na kuridhia mikataba yote ya madini na rasilimali za nchi.

 

 

 

MUSWADA WA SHERIA YA MAMLAKA YA NCHI KUHUSU UMILIKI WA RASILIMALI WA MWAKA 2017

  • Sheria inapendekeza umiliki na usimamizi wa rasilimali kuwekwa chini ya Rais na serikali. Swali ni je uwajibikaji wa serikali utakuaje?
  • Kanuni ya unufaikaji ni nzuri ili kuongeza thamani ya madini hapa nchini kabla ya kusafirishwa nje, hata hivyo tunapaswa kuwa makini na baadhi ya rasilimali kama urani ambazo zinaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii na Mazingira.

MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI WA MWAKA 2017

Jambo la kuangalia hapa ni namna gani suala la madini ambalo sio la Muungano limewekwa kwenye mikono ya Rais wa Muungano kwa niaba ya watanzania na je hili linahusisha wazanzibari?

Muswaada huu unapendekeza kuanzishwa kwa tume ya Madini na pia unataja wajumbe wa tume hiyo, ambao ni watu wawili wa heshima kwenye sekta ya madini na makatibu wakuu wa wizara husika. Mapendekezo hayajafafanua hawa watu wawili watatoka wapi. Pia tume hii inapewa mamlaka makubwa  juu ya rasimali za nchi. Tunapendekeza wajumbe wote wa tume hii wathibitishwe na Bunge ili kulinda maslahi mapana ya Nchi.

Ndugu wana habari,

Kwa kuhitimisha, HakiRasilimali inaamini kuwa sheria zinazopendekezwa kama zitaboreshwa kwa kuzingatia maoni ya wadau na kama Uwazi wa mikataba na Mapato vitasisitizwa, zitawesha Watanzania kunufaika na rasilimali zao kwa kuimarisha udhibiti na usimamizi wa uvunaji na uendelezaji wa rasilimali.

 

Imeandaliwa na Sekretarieti ya HakiRasilimali – PWYP

(Wanachama: Action for Democracy and Local Governance, Governance Links, Governance and Economic Policy Centre, Interfaith Standing committee, ONGEA, HakiMadini, Policy Forum, Tanganyika Law Society na Washirika wao Tanzania Network of Legal Aid Providers – TANLAP).

2 Julai 2017

PRESS STATEMENT-SWAHILI