June 20, 2025
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dunstan Kitandula, amesema majukwaa ya majadiliano kama Jukwaa la Uziduaji ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.Akizungumza jijini Dodoma akiwa mgeni rasmi katika kilele cha Jukwaa la Uziduaji 2025, Kitandula...
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dunstan Kitandula, amesema majukwaa ya majadiliano kama Jukwaa la Uziduaji ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.Akizungumza jijini Dodoma akiwa mgeni rasmi katika kilele cha Jukwaa la Uziduaji 2025, Kitandula alipongeza jitihada za HakiRasilimali kwa utafiti na uchechemuzi wa sera zinazohusu sekta ya rasilimali asilia, akisema mchango wa taasisi hiyo umekuwa na athari chanya kwa maendeleo ya sekta ya uziduaji nchini.
“Majukwaa kama haya yanatupa fursa ya kipekee kuunganisha nguvu kati ya serikali, wananchi, wawekezaji na mashirika ya kiraia ili kujadili kwa pamoja masuala muhimu ya sekta ya uziduaji. Hii ni njia ya kuhakikisha kuwa maendeleo tunayoyapata yanawanufaisha Watanzania wote,” alisema Kitandula.
Akiendelea kufafanua kuhusu umuhimu wa majukwaa hayo, Kitandula alisema sekta ya uziduaji imekuwa kichocheo kikuu kwa ukuaji wa sekta nyingine, ikiwemo sekta ya utalii, ambapo mikutano na matukio kama hayo huongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya asili nchini.
“Katika kipindi hiki ambacho tunalenga kuongeza mchango wa sekta ya maliasili na utalii kwenye pato la taifa, ushirikiano na sekta ya uziduaji ni wa lazima. Wakati wageni wanakuja kwa mikutano kama hii, wengi wao pia hupata fursa ya kutembelea vivutio vyetu na hivyo kuongeza mapato ya taifa,” alisema.
Kitandula pia alitumia fursa hiyo kupongeza maazimio 11 yaliyofikiwa katika jukwaa hilo, akisema yamedhihirisha namna wadau wa sekta ya uziduaji walivyo tayari kushirikiana katika kutafuta suluhu za changamoto zilizopo badala ya kulalamika tu.
Katika hotuba yake, Kitandula pia alieleza kufurahishwa kukutana tena na baadhi ya wadau na marafiki wa siku nyingi waliowahi kufanya kazi pamoja katika nyanja mbalimbali za sekta ya rasilimali.
“Nimefarijika kuwaona tena baadhi ya watu tuliowahi kushirikiana siku za nyuma. HakiRasilimali imeendelea kuwa chombo muhimu kinachoweka sekta ya uziduaji katika mstari sahihi wa maendeleo,” alisema Kitandula kwa bashasha.
Jukwaa la Uziduaji 2025 lililomalizika leo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwamo wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wawekezaji, wachambuzi wa sera na wanaharakati kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.