November 13, 2026 Updates

1. Kuimarisha Uwazi na Upatikanaji wa Taarifa za Mikataba ya Uwekezaji Serikali inashauriwa kuimarisha mifumo ya uwazi katika sekta ya uziduaji kwa kuhakikisha kuwa mikataba ya uwekezaji na taarifa muhimu zinazohusu miradi ya madini, mafuta na gesi zinapatikana kwa umma. Hali ya wananchi wa kawaida...

MUHTASARI WA MAPENDEKEZO YA WADAU WA SEKTA YA UZIDUAJI WAKATI WA KONGAMANO LA JUKWAA LA UZIDUAJI 2026
1. Kuimarisha Uwazi na Upatikanaji wa Taarifa za Mikataba ya Uwekezaji

Serikali inashauriwa kuimarisha mifumo ya uwazi katika sekta ya uziduaji kwa kuhakikisha kuwa mikataba ya uwekezaji na taarifa muhimu zinazohusu miradi ya madini, mafuta na gesi zinapatikana kwa umma. Hali ya wananchi wa kawaida kushindwa kupata taarifa za mikataba inayohusu rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao inadhoofisha ushiriki wao na uwezo wa kuhoji na kufuatilia utekelezaji wa ahadi za wawekezaji.
Ni muhimu kuweka mifumo inayowezesha wananchi, hususan jamii zinazozunguka miradi ya uziduaji, kupata taarifa kwa wakati na kwa lugha wanayoielewa. Uwazi huu utaimarisha uaminifu kati ya Serikali, wawekezaji na wananchi, sambamba na kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za taifa.

2. Kuboresha Upatikanaji wa Mitaji na Huduma za Kifedha kwa Wachimbaji Wadogo

Serikali inashauriwa kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha ili kuweka utaratibu unaowawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo na mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao. Kwa sasa, wachimbaji wengi wenye leseni wanakabiliwa na changamoto ya kupata mikopo kutokana na taasisi za kifedha kutotambua vya kutosha leseni za uchimbaji kama sehemu ya msingi wa kutathmini uwezo wao wa kupata mikopo.
Kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na mabenki na wadau wa sekta ya madini iandae mifumo rafiki ya utoaji mikopo inayozingatia mazingira halisi ya shughuli za uchimbaji mdogo. Aidha, kuwe na uwekezaji katika elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo ili kuwajengea uwezo wa kusimamia mapato, kuweka akiba, kuwekeza na kukuza biashara zao kwa uendelevu.

3. Kuimarisha Uwezeshaji wa Wanawake katika Shughuli za Uchimbaji Mdogo

Serikali inapongezwa kwa hatua zilizofikiwa katika kuwawezesha wanawake kushiriki katika shughuli za uchimbaji mdogo. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya wanawake wanaotengewa maeneo ya uchimbaji kushindwa kumudu gharama za kupata na kuendeleza leseni kutokana na ukosefu wa mitaji.
Serikali inashauriwa kuimarisha mifumo ya uwezeshaji kwa wanawake wachimbaji kupitia upatikanaji wa mitaji, teknolojia, mafunzo ya kitaalamu na huduma za kifedha. Aidha, masharti na taratibu za utoaji wa leseni zipitiwe ili kuhakikisha kuwa haziwi kikwazo kisicho cha lazima kwa wanawake na wachimbaji wadogo wenye uwezo mdogo wa kifedha kushiriki katika sekta hii.

4. Kuimarisha Ushiriki Wenye Maana wa Wananchi katika Miradi ya Uziduaji

Serikali na kampuni za uziduaji zinashauriwa kuhakikisha kuwa ushiriki wa wananchi katika michakato ya maamuzi ya miradi unakuwa wa kweli na wenye matokeo. Kumekuwa na changamoto ya wananchi kuitwa katika mikutano kwa lengo la kutimiza matakwa ya kisheria na viwango vya kampuni, bila kuhakikisha kuwa maoni na mahitaji yao yanaingizwa katika maamuzi yanayohusu miradi hiyo.
Kwa mantiki hiyo, mashauriano na jamii yanapaswa kufanyika kwa uwazi, kutoa taarifa za kutosha kabla ya maamuzi kufanyika, na kuhakikisha kuwa maoni ya wananchi yanazingatiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi. Aidha, Serikali na kampuni zinapaswa kuhakikisha kuwa mifumo ya kushughulikia malalamiko inafanya kazi kwa ufanisi, inajitegemea na inatoa majibu kwa wakati kwa wananchi walioathirika.

5. Kuboresha Mfumo wa Tathmini, Fidia na Urejeshaji wa Maisha ya Wananchi Wanaoathiriwa na Miradi

Serikali inashauriwa kuimarisha mifumo ya tathmini ya mali, ulipaji wa fidia na urejeshaji wa maisha ya wananchi wanaoathiriwa na miradi ya uziduaji. Changamoto za ucheleweshaji wa tathmini, kutokamilika kwa malipo ya fidia na athari za muda mrefu kwa maisha ya wananchi zinaendelea kuathiri ustawi wa jamii zinazopisha miradi ya uwekezaji.
Ni muhimu kuweka muda maalum na viashiria vya utekelezaji wa hatua za tathmini na ulipaji wa fidia, sambamba na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fidia stahiki kabla ya kuathiriwa na shughuli za mradi kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali iangalie upya utaratibu wa Stop Orders zinazozuia wananchi kuendeleza shughuli za kiuchumi katika maeneo yao bila kuwa na ukomo wa muda ulio wazi, ili kuepusha wananchi kuendelea kupata hasara na kuathirika kiuchumi kwa muda mrefu.

6. Kuimarisha Uhuru na Ufanisi wa Tathmini za Athari kwa Mazingira

Serikali inashauriwa kuimarisha mifumo ya tathmini za athari kwa mazingira ili kuhakikisha kuwa tathmini hizo zinafanyika kwa uhuru, weledi na kuzingatia maslahi mapana ya umma. Mfumo ambao mwekezaji ndiye anayemchagua na kumlipa mshauri anayefanya tathmini ya athari kwa mazingira unaweza kuibua changamoto za mgongano wa maslahi na kuathiri imani ya umma kuhusu uhuru na uhalisia wa matokeo ya tathmini hizo.
Kwa hiyo, Serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kufanya tathmini za kimkakati za mazingira (Strategic Environmental Assessments) katika maeneo yanayolengwa kwa uwekezaji mkubwa kabla ya miradi husika kuanza. Tathmini hizo zitasaidia kubaini maeneo nyeti kimazingira, athari zinazoweza kujitokeza kutokana na miradi mingi katika eneo moja na hatari za muda mrefu. Hatua hii inapaswa kwenda sambamba na kuimarisha usimamizi na uhuru wa tathmini za athari kwa mazingira za miradi binafsi.

7. Kuimarisha Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Maji katika Shughuli za Uziduaji

Serikali na kampuni za uziduaji zinashauriwa kuweka kipaumbele katika usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji kutokana na uwezekano mkubwa wa shughuli za uchimbaji kuathiri ubora na upatikanaji wa maji kwa jamii na mifumo ikolojia inayozunguka maeneo ya miradi.
Ni muhimu kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa matumizi na ubora wa maji, pamoja na kuanzisha au kuimarisha utoaji wa taarifa za uendelevu kuhusu rasilimali za maji (Water Sustainability Reporting). Aidha, kuwe na mifumo madhubuti ya kudhibiti na kutibu udongo na taka zenye kemikali zinazotokana na shughuli za uchimbaji kabla ya mvua kuzisomba na kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji. Hatua hizi zitasaidia kulinda afya za wananchi na kuhakikisha rasilimali za maji zinabaki kuwa salama kwa matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.

8. Kuimarisha Uratibu na Uwajibikaji wa Taasisi Zinazosimamia Sekta ya Uziduaji

Serikali inashauriwa kuboresha mifumo ya uratibu na ushirikiano miongoni mwa taasisi mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa sekta ya uziduaji. Changamoto za kutokuwepo kwa uratibu wa kutosha kati ya taasisi zenye majukumu yanayofanana zinaweza kusababisha mapungufu katika usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa sheria na kanuni.
Aidha, ni muhimu kuimarisha utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuhakikisha kuwa taasisi husika zinachukua hatua za kurekebisha mapungufu yanayobainishwa katika ripoti za ukaguzi. Uwajibikaji unapaswa kujikita katika kutatua changamoto na kuboresha mifumo ya utendaji wa taasisi, badala ya kuishia katika kubainisha mapungufu bila hatua za kuyarekebisha.

9. Kuimarisha Utekelezaji wa Local Content na Manufaa kwa Wazawa

Serikali inashauriwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera na mifumo ya Local Content ili kubaini kiwango ambacho fursa za ajira, manunuzi na huduma zinazotokana na miradi ya uziduaji zinawanufaisha wazawa, hususan jamii zinazozunguka miradi hiyo na kampuni zinazomilikiwa na Watanzania.
Tathmini hiyo izingatie pia namna ya kutambua wanufaika halisi wa fursa za manunuzi ya ndani na kubaini iwapo mifumo iliyopo inawawezesha kweli wazawa kushiriki au kama fursa hizo zinanufaisha zaidi makundi yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi. Lengo liwe kuhakikisha kuwa sera za Local Content zinachochea ukuaji wa biashara za ndani, ajira na ushiriki mpana wa wananchi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya uziduaji.

10. Kuweka Mikakati ya Kuwezesha Kampuni za Ndani Kukidhi Viwango vya ESG na Masoko ya Kimataifa

Serikali inashauriwa kuweka mikakati ya kuwawezesha wazalishaji na kampuni za ndani kukidhi viwango vya kimataifa vinavyohusiana na mazingira, jamii na utawala bora (ESG), pamoja na viwango vya uchimbaji na uzalishaji unaowajibika (Responsible Mining Standards). Ingawa baadhi ya viwango hivi ni vya hiari, kwa sasa vinazidi kuwa muhimu katika maamuzi ya wanunuzi na taasisi za kifedha kuhusu upatikanaji wa masoko na mitaji.
Hata hivyo, gharama na mahitaji ya kiufundi ya kuzingatia viwango hivyo yanaweza kuwa kikwazo kwa kampuni za ndani zenye uwezo mdogo. Kwa hiyo, Serikali inapaswa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo kutoa mafunzo, msaada wa kitaalamu na uwezeshaji wa kifedha ili kampuni za Kitanzania ziweze kuzingatia viwango hivyo na kushindana katika masoko ya kimataifa. Aidha, viwango na miongozo husika vitafsiriwe kwa Kiswahili ili kuongeza uelewa na utekelezaji wake katika ngazi za jamii na maeneo ya uzalishaji.

11. Kuimarisha Uwazi na Uendelevu wa Miradi ya CSR

Serikali na kampuni za uziduaji zinashauriwa kuimarisha usimamizi, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Miradi ya CSR inapaswa kuibuliwa kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji halisi ya jamii husika, pamoja na kuhakikisha kuwa wananchi, hususan kupitia viongozi wao wa vijiji, wanashiriki kikamilifu katika kupendekeza na kupanga miradi hiyo.
Aidha, kuwe na uwazi katika utoaji wa taarifa kuhusu fedha zinazotengwa kwa ajili ya CSR, namna zinavyotumika na matokeo ya miradi inayotekelezwa. Serikali iwawezeshe watendaji wa Serikali za Mitaa kuelewa sheria, kanuni na taratibu zinazohusu CSR ili waweze kusimamia utekelezaji wake ipasavyo. Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa miradi ya CSR inalenga kujenga uwezo wa kiuchumi na kijamii wa wananchi na kuwa na manufaa endelevu hata baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika.

12. Kuimarisha Wajibu wa Makampuni katika Kuheshimu Haki za Binadamu na Upatikanaji wa Haki

Makampuni yanayofanya shughuli za uziduaji yanashauriwa kuweka na kutekeleza sera na mifumo ya ndani ya kuheshimu haki za binadamu, kufanya tathmini za mara kwa mara za athari za shughuli zao kwa haki hizo na kuchukua hatua za kuzuia, kupunguza na kurekebisha athari zinazobainika. Wajibu huu unapaswa kuzingatiwa katika mnyororo mzima wa uwekezaji, ikiwemo kwa wakandarasi na watoa huduma kama kampuni za ulinzi. Aidha, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inashauriwa kuimarisha utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi wanaoathiriwa na shughuli za uziduaji. Makampuni nayo yanapaswa kuhakikisha ofisi na mifumo yake ya malalamiko inapatikana kwa urahisi, ikiwemo kuweka ofisi za mahusiano na jamii nje ya maeneo yenye masharti magumu ya kuingia kama ndani ya migodi. Wafanyakazi katika maeneo ya uchimbaji pia wanahimizwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuimarisha utetezi wa haki na maslahi yao.

13. Uwezo wa Wawekezaji na Mazingira ya Uwekezaji katika Madini Mkakati

Serikali inashauriwa kuimarisha mifumo ya kutathmini uwezo wa kifedha na kiufundi wa waombaji wa leseni kabla ya kutoa leseni za uchimbaji, ili kuhakikisha kuwa wana uwezo wa kutekeleza shughuli zao ndani ya muda uliopangwa. Kwa wawekezaji wa nje, uwezo wa kifedha unapaswa kuthibitishwa kwa uwazi kupitia taratibu stahiki za financial due diligence. Hatua hii itasaidia kupunguza ucheleweshaji wa miradi unaoweza kuendeleza athari kwa wananchi waliopisha uwekezaji. Aidha, Serikali na wadau wanapaswa kuweka mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa miradi ya madini mkakati kama graphite, nickel na cobalt, kwa kuzingatia changamoto zake za kipekee za kuvutia fedha za uwekezaji ikilinganishwa na madini yenye masoko yaliyoimarika zaidi kama dhahabu.

14. Kuweka Mikakati ya Uongezaji Thamani wa Madini Inayozingatia Uwezo Halisi wa Nchi

Serikali inashauriwa kuweka mikakati mahususi ya uongezaji thamani wa madini kwa kuzingatia sifa za kila aina ya madini, mahitaji ya teknolojia, upatikanaji wa nishati na gharama za uwekezaji katika kila hatua ya mnyororo wa thamani. Badala ya kuweka matarajio ya jumla ya kuchakata madini yote hadi kufikia bidhaa za mwisho, ni muhimu kufanya uchambuzi wa gharama na manufaa (cost-benefit analysis) ili kubaini hatua ambazo Tanzania inaweza kuanza kutekeleza kwa ufanisi na kwa kuzingatia uwezo wake wa sasa. Kwa mfano, uchakataji wa madini kama nickel, cobalt na graphite unahitaji uwekezaji mkubwa wa nishati na teknolojia. Hivyo, ni muhimu kuwekeza katika miundombinu ya nishati na teknolojia na kuweka mpango wa hatua kwa hatua wa kuongeza kiwango cha uchakataji ndani ya nchi.

Related Posts

Hon. Dunford Mpelumbe Officially Opens Jukwaa la Uziduaji 2026 in Dodoma
Nov 12, 2026

Hon. Dunford Mpelumbe Officially Opens Jukwaa la Uziduaji 2026 in Dodoma

The Guest of Honour, Hon. Dunford Mpelumbe, officially opened Jukwaa la Uziduaji 2026 in Dodoma, marking the beginning of a two-day platform for dialo...

JUKWAA LA UZIDUAJI 2026
Oct 19, 2026

JUKWAA LA UZIDUAJI 2026

HakiRasilimali is pleased to announce Jukwaa la Uziduaji 2026, taking place on 12–13 November 2026 in Dodoma, Tanzania. Under the theme “From Natural...