Imeelezwa kuwa Serikali ikishirikiana na Asasi za kiraia itafanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanikisha kutekeleza malengo ya Dira ya madini ya Africa.

Hayo yamebainishwa leo, Oktoba 25, 2021 jijini Dodoma na Mjumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jesca Kishoa katika mjadala wa wazi wa wiki ya Azaki kuhusu usimamizi endelevu wa sekta ya madini kwa maendeleo jumuishi.

Kishoa amesema kuwa moja ya changamoto iliyopo ni serikali kulibeba swala la Dira ya madini ya Afrika peke yake pasipo kushirikisha wadau ambao wanaweza kutoa maoni na michango chanya inayoweza kuleta tija katika Dira hiyo.

Sambamba na hayo Kishoa amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupewa Elimu na Asasi za kiraia kuhusu umuhimu wa Rasilimali za nchi katika kuwanufaisha wananchi wenyewe pasipo kutegemea Serikali peke yake.