Imeelezwa kuwa gesi ya Helium inayotarajiwa kuzalishwa katika bonde la Ziwa Rukwa mkoani Rukwa ina uwezo wa kuuzwa kwenye soko la dunia kwa miaka 20 ijayo.

Hayo yameelezwa leo na Mbunge wa jimbo la Kwela wilayani Sumbawanga, Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma alipotembelea banda la HakiRasiliamali katika wiki ya Azaki 2021.

Mhe. Sangu amesema kuwa Mkoa wa Rukwa una utajiri mkubwa wa gesi ya Helium na kwamba mara baada ya mradi kukamilika gesi hiyo italiingizia kipato kikubwa taifa kutokana na uuzaji wake katika soko la dunia.

Ameongeza kuwa kwa sasa Marekani ndiyo inayoongoza katika uuzaji wa gesi ya Helium na kwamba mara baada ya kukamilika mradi huo wa Bonde la Rukwa Tanzania itaingia katika soko la dunia kuuza rasilimali hiyo.

Sambamba na hayo Mhe. Sangu ameiomba Wizara ya Nishati kufanya ziara za mara kwa mara mkoani Rukwa ili kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha ili watambue umuhimu wa gesi hiyo na faida zake kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Mhe. Sangu amebainisha changamoto zilizopo kwa sasa katika mradi huo kuwa ni pamoja na ubovu wa barabara, ushirikishwa wa wananchi, pamoja na wazawa kukosa ajira ndogondogo ambazo zinatolewa kwa watu kutoka nje ya maeneo ya mradi.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa asasi ya HakiRasilimali Rachael Chagonja amesema kuwa rasilimali za nchi ni vyema zikawanufaisha wananchi wenyewe na kwamba elimu itolewe kwa wananchi ili kila mmoja afahamu utajili wa rasilimali katika eneo analoishi.

Mradi wa gesi ya Helium katika bonde la ziwa Rukwa umeanza mwaka 2016; una mita za ujazo zipatazo bilioni 98; na kwa sasa upo katika hatua za awali za ujenzi.