Na HakiRasilimali

Wadau wa sekta ya madini nchini wameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli kwa hatua yake ya kutangaza kwamba itanunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo ikiwa lengo ni kunusuru biashara zao zilizoathirika kutokana na ugonjwa wa corona (Covid-19).

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Stanslaus Nyongo hivi karibuni alisema kwamba serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) imeamua kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuendelea na shughuli zao za uchimbaji pamoja na changamoto ya wanunuzi wa nje baada ya nchi nyingi kufunga mipaka yao kipindi hiki cha ugonjwa wa Covid-19 ulioathiri jumla ya nchi 213 duniani.

“Kwa niaba ya wachimbaji wenzangu wanawake, napenda kuishukuru serikali kwa kusikia kilio chetu cha ukosefu wa masoko kipindi cha ugonjwa huu wa corona. Tuna imani hii itatusaidia sisi kujikimu na mambo mbalimbali na kutufanya tuendelee na kazi na kulipa kodi kwa serikali,” anasema Salma Kundi, Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA).

Anaongeza kwamba: “Tunampongeza sana Rais wetu Magufuli, Wizara ya Madini na Stamico kwa kuendelea kutujali wachimbaji wadogo. Haijawahi kutokea kwa serikali zilizopita kutujali wachimbaji wadogo kwa kiwango hiki.”

Nae kwa upande wake Amani Mhinda, Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia ya HakiMadini ambayo inajishughulisha na usimamizi wa haki ya wachimbaji wadogo wa madini na jamii inayozunguka maeneo ya uchimbaji nchini, ameipongeza serikali kwa hatua ya kununua dhahabu lakini pia ameshauri kwamba biashara hiyo iwe ya kimkakati na endelevu ili iwanufaishe wachimbaji wadogo na serikali kama ilivyokusudiwa.

“Ununuzi na uuzaji wa dhahahu ni biashara kama biadhara zingine, kwa hivyo watakaokuwa wanasimamia biashara hiyo wawe na uelewa wa mwenendo mzima wa masoko ya dunia ili kuwezesha serikali kupata faida, na wachimbaji kunufuika kwa kuuza kwa bei nzuri,” amesema Mhinda.

Pia ameishauri serikali kujifunza kutoka kwa nji ya Ethiopia ambayo kwa takribani miaka mitano (5) imekuwa inanunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji, na kuweza kuinua uchumi wake kupitia biashara ya dhahabu.

Kwa upande wake, Lucy Shao, ofisa programu wa asasi ya kiraia ya HakiRasilimali inayojishughulisha na masuala ya uchimbaji madini, mafuta na gesi nchini amesema,”Ni hatua nzuri na ya kupongezwa, kwani hata zamani Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilikuwa inanunua dhahabu na kuiweka na badae kuiuza nje ya nchi kwa bei nzuri.”

Pia ameishauri serikali kupitia Wizara ya Madini ione haja ya kununua madini ya vito kama Almasi, Tanzanite, ikiwa lengo ni kuwawezesha kiuchumi wachimbaji wa madini nchini waweze kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na ugonjwa wa corona.

Tangia mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 utokee nchini mwezi March mwaka huu, sekta nyingi za uchumi zimeathirika ikiwamo Sekta ya Madini ambapo kutokana na hofu ya maambukizi ya ugonjwa huu hatari ulioanzia China mwezi Disemba, 2019, baadhi ya makampuni makubwa na madogo ya madini nchini yalilazimika kusitisha zoezi la uchimbaji. Hali ambayo imeathiri ajira za maelfu ya wafanyakazi na kuikosesha serikali mapato kupitia kodi.

Kutokana na hali ya biashara ya madini nchini kuzidi kuwa mbaya, wadau wa sekta ya madini nchini waliiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kunusuru biashara hiyo hususani kuwawezesha wachimbaji wadogo ambao kwa kiasi kikubwa ndio wameathirika zaidi kutokana na ukosefu wa masoko ya kimataifa uliosababishwa na hatua ya nchi za nje kuweka zuio la kusafiri ikiwa lengo ni kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi zao.

Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya madini yanayozalishwa nchini hutegemea masoko ya kimataifa ambapo huuzwa nchini Ujerumani, Marekani, China na nchi zingine.

Mwisho-