Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti Omary Kigau amesema Asasi za Kiraia nchini zina mchango mkubwa katika mapato ya nchi, ajira na upangaji wa Bajeti.

Kigau ambaye ni Mbunge wa jimbo la Kilindi Mkoani Tanga amesema hayo leo Oktoba 23, 2021 alipotembelea banda la Taasisi ya HakiRasilimali katika maonyesho ya wiki ya Azaki 2021 ambayo kauli mbiu yake ni Azaki na Maendeleo.

“Katika nchi yetu tuna changamoto ya upungufu wa ajira, Vijana wanaomaliza Vyuo Vikuu ni wengi na Serikali haiwezi kuwaajiri wote lakini wapo ambao wanaajiriwa na asasi hizi,” amesema Kigau.

Kwa upande wa bajeti Kigau amesema waajiriwa wa asasi hizo wanalipa kodi kama Paye, VAT na Withholding lakini pia Asasi kama HakiRasilimali hutoa maoni yao ya nini kifanyike katika upangaji wa bajeti.