Jukwaa la Uziduaji la mwaka 2025 limezinduliwa rasmi leo katika Ukumbi wa Mabeyo Complex jijini Dodoma, likiwakutanisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kujadili hali ya sasa na mustakabali wa sekta ya uziduaji nchini Tanzania.

Likiratibiwa na shirika la HakiRasilimali, jukwaa hilo la siku tatu linafanyika kuanzia leo Juni 17, 2025 chini ya kaulimbiu isemayo: “Hali na Mustakabali wa Sekta ya Uziduaji: Uwekezaji Wenye Kuwajibika na Mpito wa Nishati.”

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiRasilimali, Adam Anthony, amesema jukwaa la mwaka huu litajikita kwenye maeneo saba muhimu ya majadiliano ambayo ni ya msingi kwa maendeleo ya sekta hiyo.

“HakiRasilimali ni mtandao wa mashirika ya kiraia 19, na tumekuwa tukiandaa jukwaa hili kwa zaidi ya muongo mmoja. Limekuwa ni jukwaa la kitaifa linalowakutanisha wadau kubadilishana mawazo na kupendekeza suluhisho kwa ajili ya ukuaji endelevu na shirikishi katika sekta ya uziduaji,” amesema.

Ameeleza kuwa jukwaa hilo limekuwa likichangia matokeo chanya katika sekta hiyo kwa kuwezesha majadiliano kati ya watunga sera, wawakilishi wa jamii, wadau wa sekta binafsi na mashirika ya kiraia.

Kwa mwaka huu, jukwaa litajadili mustakabali wa Sekta ya Madini Tanzania, Siasa za ulimwengu kuhusu Madini ya Mpito na Mwelekeo wa Uwekezaji Afrika, Uendeshaji Biashara kwa Uwajibikaji katika Madini ya Mpito, fursa za uchimbaji mdogo pia jukwaa hili litatumika kutafsiri uwazi na uwajibikaji katika sekta madini na hali ya usimamizi wa Rasilimali nchini Tanzania.

Share This Story, Choose Your Platform!

continue reading

Related Posts